Jumamosi 24 Oktoba 2026 - 16:38
Jinsi ya Kuufafanua Upya Mwenendo wa Bibi Fatima Zahra (as) kwa Wasichana na Wanawake wa Leo?

Hawza/ Bila shaka, mwenendo na maisha ya Bibi Fatima Zahra (sa) ni mfano bora kabisa wa ustahimilivu kwa binadamu katika nyanja za mtu binafsi na kijamii, hususan kwa wanawake na wasichana wa jamii.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika siku hizi za kukumbuka shahada ya kusikitisha ya Bibi Fatima Zahra (sa), tumefanya mahojiano na Dkt. Masoumeh Nasiri, mhadhiri na mtafiti wa elimu ya vyombo vya habari, yafuatayo ni maelezo kamili ya mahojiano hayo.

Swali:

Katika zama za kuenea utamaduni wa matumizi ya kupita kiasi na kujionesha kupitia vyombo vya habari, tunawezaje kuufafanua upya mwenendo wa Bibi Fatima Zahra (sa) kama mfano unaowajengea utambulisho wasichana na wanawake wa leo, katika njia ya kufikia saada na mafanikio yao duniani na Akhera?

Jawabu

Umebainisha jambo muhimu sana kupitia swali hili. Ukweli ni kwamba tunaishi katika zama ambazo kwa masikitiko, tunashuhudia mtazamo unaomchukulia mwanamke kama kitu cha kutumiwa. Suala hili limepata maana na nafasi yake ya pekee katika kipindi hiki cha kuenezwa utamaduni wa matumizi ya kupita kiasi.

Hata hivyo, napenda kusema kwamba mimi si miongoni mwa wale wanaounga mkono sana mtazamo wa kulizungumzia suala hili kwa kuzingatia tu maisha rahisi ya Bibi Fatima (sa). Badala yake, tunapaswa kuuchukulia mwenendo wa Bibi huyu mtukufu, ambaye ni “Sayyidatu Nisaa al-Aalamin” (Kiongozi wa Wanawake wa Ulimwengu), kuwa ni mfumo wa kimawazo na uti wa mgongo wa fikra za madhehebu ya Shia. Tunapaswa kuzingatia vipengele vyake na kuvifafanua kwa usahihi kwa jamii nzima ya binadamu, wala si kwa jamii yetu pekee.

Bila shaka, tunapoitazama shakhsia hii kubwa kihistoria, kidini na kibinadamu kwa mtazamo huu, katika hatua inayofuata tutakuwa na njia bora na sahihi zaidi ya kuwasilisha mifano inayowajengea watu utambulisho, njia hiyo itatuwezesha kufikia lengo letu.

Jambo lililo wazi ni kwamba Bibi Fatima (sa) alikuwa na vipengele mbalimbali vya maisha yenye mafanikio katika nyanja za kijamii, kiutamaduni na malezi. Kipengele ambacho, kwa mtazamo wangu kinaweza kuzingatiwa kama mfano wa kujenga utambulisho na ambacho tunaweza kukipa uzito katika kuunda mifano ya kuigwa, ni uwezo wa kutambua mazingira na nafasi, kufahamu zama husika, pamoja na kufafanua nafasi tofauti ya kijamii na ile inayotokana na imani na mitazamo iliyozoeleka katika jamii.

Haya ni miongoni mwa mambo ambayo Bibi Siddiqah Kubra (sa) aliyazingatia katika zama zake, na kwa namna fulani akatekeleza jukumu hili muhimu ambalo linatoa mfano wa kuigwa.

Ni muhimu kwa wanawake na wasichana wetu kutambua kwamba, mambo yanayopata nguvu na kutawala kupitia vyombo vya habari, pamoja na mitindo mbalimbali ya maisha inayozidi kuenea, ndiyo tunayoyaita leo utamaduni wa matumizi ya kupita kiasi na kujionesha. Kwa mtazamo wangu, tukiyachunguza maisha ya Hazrat Fatima (sa) kwa umakini na kwa kina, tutaona kwamba alikuwa akisimama kupinga mambo yaliyokuwa na ushawishi hasi katika jamii, alijitahidi kuishi na kuendesha maisha yake kwa namna inayolenga kumwabudu Mwenyezi Mungu, kusimamisha haki na kutetea wilaya.

Iwapo tutafanikiwa kuwajengea wasichana wetu ujasiri na uthubutu wa kuelewa kwamba si kila jambo linaloelekezwa au kuamriwa na jamii linamaanisha kuwa ni sahihi na la kweli, tutakuwa tumepiga hatua muhimu. Vilevile, wanapaswa kuelewa namna ya kuchagua maisha bora zaidi bila kuathiriwa na mitazamo na fikra zinazotawala katika jamii ya zama zetu, kwa mtazamo wangu, suala hili linaweza kuwa mojawapo ya michakato muhimu ya kufikia lengo hilo.

Kwa hiyo, kulizungumzia suala la maisha rahisi ya Bibi Fatima (sa) pekee, kwa maoni yangu, ni kupunguza upeo wa uwezo na ukubwa wa shakhsia yake. Hii ni kwa sababu alikuwa na vipengele mbalimbali vya kiutu, shakhsia, kiroho na kimaanawi, vipengele hivi vinapaswa kufafanuliwa kwa usahihi kwa lugha inayoendana na mahitaji ya zama hizi, ili viweze kueleweka na umma kwa ujumla, hususan wanawake na wasichana vijana.

Swali:
Kwa kuzingatia mwenendo wa Bibi Fatima (sa), dhana ya “haya” inaonekana kuwa ni zaidi ya suala la aina ya mavazi, bali ni “muundo wa ndani ya nafsi.” Kwa mtazamo wako, dhana hii inawezaje kuwa ngao ya kujilinda dhidi ya migogoro inayolenga kufuta utambulisho na kuporomoka maadili katika anga za mtandaoni?

Jawabu:
Angalia, suala la haya au kuwa na heshima na kujiepusha na mambo yasiyofaa linahusiana na mavazi. Hata hivyo, ni lazima tufahamu kwamba kuvaa mavazi yanayofunika mwili hakumaanishi moja kwa moja kuwa mtu ana haya na anajisitiri kwa maana pana ya maadili. Hapa ndipo linapojitokeza swali: Ni kwa namna gani mambo haya mawili yanaunganishwa?

Katika kujibu swali hilo, tunapaswa kusema kwamba, hali hii hujengwa kupitia mfumo wa malezi na muundo wa ndani ya nafsi unaotokana na mafunzo hayo ya malezi. Yaani, mtu anajisitiri kwa mavazi, na wakati huohuo anajizuia kimaadili na kuwa na haya, hili ni jambo muhimu sana ambalo, angalau, tunapaswa kulipa uzito.

Suala la kujizuia kimaadili na haya, pamoja na suala la mavazi, linahusiana na uimara wa hali ya kujithamini ndani ya watu katika jamii, katika muktadha huu tunawazungumzia wanawake.

Swali ni hili: Tunawezaje kuwa na hali imara ya kujithamini? Ni hali hii ya kujithamini inayoungana na vipengele vya haya, kujisitiri kimaadili na mavazi, na ambayo inaweza kuwa ngao ya kujilinda. Kwa hakika, inaweza pia kuwa kipengele muhimu cha kukabiliana na dhana mpya zinazojengwa kuhusu utambulisho, Hata hivyo, katika suala hili mimi nitaacha kuendelea kujadili dhana ya kufutwa utambulisho.

Kwa vyovyote vile, anga za mtandaoni zimegeuka kuwa mahali au alama ya kudhihirika tabia zisizo na kujizuia kimaadili na vitendo vinavyopunguza au kuondoa haya.

Jinsi ya Kuufafanua Upya Mwenendo wa Bibi Fatima Zahra (as) kwa Wasichana na Wanawake wa Leo?

Kwa mtazamo wangu, iwapo tutaweza kusimamia na kuimarisha vipengele vya kisaikolojia kama vile hali ya kujithamini, sambamba na dhana za kujizuia kimaadili, mavazi ya staha na haya, basi tutaweza kudhibiti kwa urahisi utambulisho mpya unaojengwa na kuundwa kupitia vyombo vya habari, pamoja na mambo yanayopinga mfumo wa maadili.

Sawali:
Kwa maoni yako, tunawezaje kutumia mfano wa kitabia wa Bibi Fatima (sa) katika kukabiliana na changamoto za maisha ili kuimarisha “ustahimilivu wa kijamii” miongoni mwa kizazi kipya? Aidha, mazungumzo na ujumbe tunaoujenga kupitia vyombo vya habari, hususan katika kufafanua na kueneza fikra hizi kwa kuongozwa na mwenendo na mtindo wa maisha ya Kifatimiyya, yanapaswa kuwa ya namna gani?

Jawabu:
Katika kujibu swali hili, jambo linalonijia akilini ni kwamba Bibi Fatima Zahra (sa) ni mfano kamili wa muqawams na ustahimilivu. Bila shaka, ustahimilivu huu hujengwa kutokana na kipengele cha kimawazo na kimalezi, pamoja na imani thabiti ya ndani ya nafsi.

Kwa vyovyote vile, yeye ni binti wa Mtume Mtukufu wa Uislamu; Mtume aliyeleta dini na kuanzisha dini hiyo. Bibi Fatima (sa) alikuwa karibu sana na kitovu cha matukio na mabadiliko yaliyotokea katika kipindi chote cha maisha ya kisiasa ya baba yake mtukufu, na yeye mwenyewe aliyashuhudia na kuyapitia matukio hayo.

Katika maisha yake pamoja na Imam Ali (as), na alipokabiliana na maadui wa Uislamu na Wilaya ambao kwa kushangaza, walikuwa na mizizi ndani ya mifumo ya Kiislamu, au angalau walikuwa wakijionesha kwa sura ya Kiislamu, tulishuhudia matukio mbalimbali kama vile suala la Fadak, Saqifa na mengineyo.

Katika matukio hayo, tunaona waziwazi ustahimilivu katika maisha yake, iwe katika nyanja za kijamii, kifamilia au hata kiuchumi.

Kwa hiyo, ni muhimu kwa wanawake wetu kuwa na ufahamu sahihi kuhusu mtindo wa maisha ya Bibi Fatima (sa). Hasa wanapaswa kufahamu kwamba ili mtu aendelee kukumbukwa katika historia, ni lazima awe na ustahimilivu, ni ustahimilivu huu unaomfanya mtu kuwa shakhsia inayokumbukwa na jamii kwa muda mrefu.

Kwa mtazamo wangu, wanawake watakapolielewa jambo hili, wataanza kulitambua jukumu lao kwa namna tofauti.

Kwa vyovyote vile, mfumo huu wa malezi ulizaa watu wakubwa na mashuhuri kama vile Imam Hassan (as), Imam Hussein (as) na Zainab Kubra (as), ambao waliwasilishwa kwa jamii ya binadamu.

Kwa hiyo, huu ni mfumo sahihi na kamili kabisa. Ustahimilivu maana yake ni kusimama imara katika misingi ya kanuni, kuendelea kutembea katika njia ya haki na ukweli. Bila shaka, ni upinzani na msimamo wake huu ambao hatimaye ulisababisha shahada yake ya kusikitisha huku akiwa amedhulumiwa.

Jambo muhimu ni kwamba tunapaswa kufafanua vipengele mbalimbali vya mwenendo na maisha ya Bibi Fatima (sa), pamoja na athari za muda mrefu za ustahimilivu wake kwa wanawake.

Tunapaswa kufafanua namna mwanamke kwa kuwa tu mwanamke, anavyoweza kuifanya jamii kuwa yenye ustahimilivu kupitia ustahimilivu wake mwenyewe, na pia kuijenga familia yenye ustahimilivu.

Vilevile, tunapaswa kuelewa namna uwezo wa mwanamke kutambua mazingira na nafasi yake katika matukio ya kihistoria unavyoweza kumwezesha kujenga na kupanua mazingira imara, muhimu na yenye nguvu katika jamii. Kwa maoni yangu, tumefanya kazi ndogo katika eneo hili.

Bibi Fatima (sa) ni miongoni mwa wanawake wachache sana waliokuwa mstari wa mbele katika historia. Yaani, wakati ambapo kulikuwa na hali ya ukimya wa watu wengi dhidi ya Amirul-Muuminin (as), na kwa hakika dhidi ya Uislamu na wilaya, yeye alisimama imara na kuvunja ukimya huo.

Mahali ambapo ilihitajika kuchukua hatua za moja kwa moja katika uwanja wa matukio, alifanya hivyo. Mahali ambapo ilihitajika kutoa ufafanuzi na kuelimisha watu, alifanya hivyo. Na mahali ambapo ilihitajika kunyamaza kwa busara na kwa msingi wa elimu, alifanya hivyo pia.

Alitekeleza wajibu na jukumu lake kwa usahihi na kwa namna inayostahili.

Kwa hiyo, kuelewa mazingira haya na kutambua nafasi ya matukio katika kila kipindi kunaweza kutusaidia sana kutumia mwenendo wake kama mfano wenye uwezo wa kujenga na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Mahojiano na: Sayyid Muhammad Mahdi Mousavi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha